Mawakili watakiwa kutambua fursa za ajira

0
193

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema changamoto ya ajira katika kada ya sheria duniani ni kubwa, na hivyo amewataka Mawakili wapya nchini kuendelea kujifunza na kutambua fursa za ajira zinazoletwa na mabadiliko ya teknolojia duniani.

Jaji Mkuu amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa Sherehe ya 68 ya Kuwakubali na Kuwapokea Mawakili wapya zaidi ya 100.

Amesisitiza kuwa Mawakili wanapaswa kutambua fursa ambazo wengine bado hawajaziona.

Profesa Juma amebainisha kuwa mizani ya ajira imebadilika kutoka Ile ambayo wahitimu wa vyuo vikuu walikuwa wakifuatwa ili wakachague kazi wanayotaka tofauti na hivi sasa ambapo kila kijiji kina mhitimu wa Chuo Kikuu na hana ajira.

“Mawakili wapya mnapaswa kujua mabadiliko yanayotokea kwenye jamii sio tu Tanzania bali duniani kote ambayo yamechangia kuondoa ajira za kudumu ambazo tumezizoea kutokana na matumizi makubwa ya teknolojia.” Amesema Jaji Mkuu

Aidha amevitaka vyuo vinavyotoa mafunzo ya sheria nchini kuhakikisha vinatoa masomo mapana yanayoweza kuwafanya wale wanaopata shahada waweza kuajirika.

Pia Jaji Mkuu amewataka Mawakili hao kutambua fursa za ajira zinazotokana na Uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali kwenye miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).

“Wenzetu ambao ni Mawakili kama ninyi kutoka mataifa mengine wanaposikia kuna uwekezaji mkubwa kama huu ambao unaunganisha nchi yetu na nchi zingine wao wanaona ni fursa, hivyo ni wakati wenu kuvaa miwani itakayowafanya kutambua fursa zilizopo kwenye miradi kama hii”. Ameongeza Jaji Mkuu wa Tanzania