Kiwanda cha kuchakata mahindi chazinduliwa Mlale

0
258

Rais John Magufuli amezishauri Taasisi mbalimbali nchini kulipa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kazi za dharula zinazojitokeza zikiwemo zile za ujenzi wa barabara na madaraja pamoja na uokoaji kwa kuwa majeshi hayo yamekua yakifanya kazi hizo kwa haraka na kwa ufanisi.

Rais Magufuli ametoa ushauri huo mkoani Ruvuma,  mara baada ya kuzindua kiwanda cha kuchakata mahindi kilichopo katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Mlale, kiwanda  kilichojengwa na JKT kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Milioni 400.

Amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania  na Jeshi la Kujenga Taifa kwa uharaka wa kufanya kazi mbalimbali na kwa ufanisi, hata kwa kazi ambazo zilidhaniwa kuchukua muda mrefu.

Rais Magufuli pia amewapongeza askari wote wanaofanya kazi katika kiwanda hicho cha kuchakata mahindi kilichopo katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Mlale kwa kuwa wanafanya kazi nzuri na ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika kuifanya kazi hiyo.

Ametoa wito kwa Wawekezaji mbalimbali nchini  kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao hasa mahindi,  ili kuzuia kupotea kwa mazao hayo kabla ya kuchakatwa.

Awali, Mkuu wa  Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo alimshukuru Rais Magufuli kwa kuzindua kiwanda hicho ambacho ni muhimu kwa kumkomboa mkulima ambaye mazao yake mengi yalikua yakiozea shambani, ambayo kwa sasa yatafikishwa kiwandani hapo na kuchakatwa.

Jenerali Mabeyo amesema kuwa JWTZ na JKT wataendelea kuanzisha viwanda mbalimbali vitavyotumia rasilimali zilizopo nchini,  ambavyo vitaongeza ajira na pia kuchangia uchumi wa nchi.

Amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa Jeshi litaendelea kufuata maelekezo na maagizo mbalimbali yanayotolewa na serikali, maagizo yenye lengo kuleta ustawi kwa Taifa.

Rais John Magufuli anaendelea na ziara yake ya siku Sita mkoani Ruvuma.