Mabasi ya New Force yapigwa ‘stop’ kusafiri alfajiri

0
141

Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imesitisha ratiba za mabasi 38 ya kampuni ya mabasi ya New Force yanayoanza safari kuanzia saa 9 na saa 11 alfajiri.

LATRA imefikia uamuzi huo kufuatia kutokea kwa ajali tano hivi karibuni zilizohusisha mabasi ya abiria yanayomilikiwa na kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa LATRA, ajali hizo zimetokea ndani ya kipindi cha wiki nne na kusababisha madhara kwa abiria.

Mkurugenzi wa LATRA, Habibu Saluo amewaambia waandishi wa habari kuwa, kutokana na kuwepo kwa ajali nyingi kwa kipindi kifupi zilizohusisha mabasi ya kampuni ya Mew Force, walifanya uchunguzi na kubaini uvunjaji wa sheria kwa makusudi wa kanuni za usafirishaji wa magari.

“Kampuni ya New Force ni miongoni mwa watoa huduma waliopewa ratiba za saa 9:00 alfajiri mabasi 10 na saa 11:00 alfajiri mabasi 28 na walipewa sharti la kuhakikisha sheria zinazingatiwa lakini kwa makosa haya tunasitisha ratiba yao”. amesema Saluo.

Amesema kuanzia Julai 05, 2023 mabasi hayo yatafanya safari zake kuanzia saa 12 asubuhi.