Bunge laridhia marekebisho ya mipaka ya Hifadhi ya Ruaha

0
301

Bunge la Tanzania leo limepitisha maazimio mawili ambayo moja ni, Azimio la Kuridhia Kufanyika Marekebisho ya Mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, pili ni, Azimio la Kuridhia Kufutwa kwa Hifadhi ya Taifa Kigosi ili kuruhusu Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Kigosi.

Serikali imeona ni vema kufuta Hifadhi ya Taifa Kigosi ili kuruhusu kuanzishwa kwa Hifadhi ya Msitu Kigosi ambao utasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) ambapo pamoja na mambo mengine itatoa fursa kwa wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwenye eneo hilo kwani sheria inaruhusu kufanyika shughuli hizo ndani ya hifadhi za misitu kwa kuzingatia matakwa ya uhifadhi na utaratibu maalum.

Aidha, uamuzi wa kurekebisha mipaka utakuwa na manufaa mbalimbali ikiwemo kutoa eneo lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 478 ambalo litamegwa kutoka kuwa sehemu ya hifadhi kwenda kwa wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo na ufugaji katika vijiji 29.

Aidha, manufaa mengine ni kutunza vyanzo vya maji na kuboresha mifumo ya ikolojia katika Bonde la Usangu, kuimarisha uhifadhi wa maliasili, kuondoa migogoro ya mipaka, kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika Pato la Taifa na kuwezesha upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli nyingine za kiuchumi.