Waandishi wa habari sita wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wameteuliwa kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) za mwaka 2022, zitakazotolewa Julai 22, 2023 mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza katika halfa ya kuwatangaza wateule hao jijini Arusha, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga amesema, kumekuwa na ongezeko kubwa la waandishi wa habari kutuma kazi zao kutoka kazi 598 zilizotumwa mwaka 2021 hadi kazi 893 zilizotumwa mwaka 2022.
Kwa upande wake Jaji Mkuu Mkumbwa Ally aliyeongoza jopo la majaji sita kupitia kazi hizo amesema, ubora wa kazi umeongezeka hususani kazi za vyombo vya mitandaoni huku akitoa rai kwa wahariri kusaidia kuongeza ubora wa kazi za waandishi kwa kuhakikisha wanafuata vigezo vyote vya uandishi wa habari.
Waandishi hao wa habari wa TBC walioteuliwa ni Ezekiel Shamakala, Anna Peter, D’jaro Arungu, Peter Lugendo, Ahmad Ally, na James Lerombo.
Majaji wengine walioshiriki katika uteuzi wa kazi hizo ni pamoja na Mwanzo Millinga, Peter Nyanje, Mbaraka Islam, dkt. Egbert Mkoko, Rose Mwalimu na Nasima Haji Chum.