Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkuu wa mkoa wa Mbeya, Juma Homera na Kamati ya Usalama ya mkoa huo wafanye uchunguzi zaidi na kwa haraka kuhusiana na tukio la kupotea kwa Mwanafunzi Esther Noah wa shule ya sekondari ya Panda Hill mkoani humo.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya kupokea ‘clip’ yenye maelezo ya mzazi wa binti huyo ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano, tahsusi ya PCB kwenye shule hiyo.
Katika ‘clip’ hiyo, Mama yake Esther amedai kwamba yeye na mume wake waliitwa na uongozi wa shule hiyo na kujulishwa kwamba Esther hajaonekana tangu asubuhi ya Mei 18, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.
Mama Esther amedai kuwa Esther aliacha ujumbe wa maandishi akiwaaga rafiki zake na kuomba Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu.
“Naomba umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya maisha yangu mimi kuwa magumu,” amedai Mama yake Esther akisoma sehemu ya ujumbe huo wa mtoto wake.