Za ndaaani, Mayele harudi Yanga – Babu Tale

0
450

Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu Babu Tale amesema taarifa za ndani, zinaeleza kuwa mshambuliaji wa Yanga SC, Fiston Mayele hatorudi kwenye klabu hiyo msimu ujao.

Babu Tale amesema hayo akimtania Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akichangia bajeti ya serikali kwa mwaka 2023/24 ambapo amemtaka waziri huyo kuhakikisha anakuza sekta ya michezo.

Mbunge huyo amesema kama Mwigulu ambaye anapenda michezo yupo wizarani na bado sekta ya michezo inazorota, anaamini kwamba kwamba akiondoka, sekta hiyo itakuwa kwenye hali mbaya zaidi.

“Lakini waziri, kaka yangu, mwanamichezo tunayekutegemea, ingawa timu yako imehsapoteza kocha, na hivi karibuni, za ndaaaani, Mayele harudi, naona wazi utakwenda kuisaidia wizara,” amesema Taletale.

Kwa mara nyingine ameendelea kuisisitiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhamishia michezo ya kubahatisha kwenye Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuiwezesha kupata fedha za kutosha zitakazowezesha kukuza sekta hiyo iliyoajiri vijana wengi.

“Siku ya wewe kufungua moyo kuichukua michezo ya kubashiri kuipeleka wizara ya michezo ndio siku ya wizara hii ya michezo kwenda kusaidia michezo na sanaa kwa uhakika,” amehitimisha huku akikataa kuunga mkono hoja hadi atakaposikia majibu ya waziri.