Utafiti wa Nguvukazi na Ajira wa mwaka 2020/21 umebaini kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Tanzania kimekuwa na mwenendo wa kupungua katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imeeleza.
Kwa mujibu ripoti ya Hali ya Uchumi mwaka 2022 ukosefu wa ajira nchini Tanzania kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 ulipungua hadi asilimia 9.3 kutoka asilimia 10.5 mwaka 2014.
Kwa mujibu wa utafiti huo, kupungua kwa kiwango hicho ni matokeo ya juhudi mbalimbali zilizotekelezwa na Serikali, ingawa viwango vya ukosefu wa ajira bado ni vya juu na vinahitaji juhudi zaidi kuvipunguza.
Aidha, hali ya ukosefu wa ajira kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 nchini Tanzania imekuwa ikiongezeka kutoka asilimia 12.1 mwaka 2014 hadi asilimia 12.6 mwaka 2020/21.
Utafiti umebaini kuwa tatizo hili ni kubwa zaidi kwa vijana wa kike (asilimia 16.7) ikiwa ni mara mbili ya kiwango kwa vijana wa kiume (asilimia 8.3).
Akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali mwaka 2023/24 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Ncemba alisema “jawabu la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuondoa umaskini kwa Watanzania ni kukuza uwekezaji, hususani katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi,” hatua ambayo Serikali itachukua.