Wabunge wataka wanaojifungua watoto njiti kuongezewa likizo

0
265

Serikali imewataka Wabunge kutoa maoni endapo kuna haja ya kurekebisha Kanuni za Utumishi wa Umma kuhusu likizo kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti ili wapate muda wa kutosha wa kulea watoto hao wanaohitaji uangalizi wa karibu.

Rai hiyo imetolewa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene alipokuwa akijibu swali na kuongeza kuwa kwa sasa kanuni zinatoa siku 84 za likizo ya uzazi kila baada ya miaka mitatu, lakini mzazi anaweza kuongezewa muda endapo anaumwa au dharura nyingine ya kiafya.

“Sasa tutajaribu kuona kama inatosha au haitoshi kwa sababu mtu anapozaliwa akifariki inaumiza sana. Na wengi humu tumezaliwa tukiwa njiti, hatujisemi tu, tusingeangaliwa kwa siku zaidi ya 84 tusingekuwa humu,” amesema Waziri Simbachawene

Akiuliza swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalum, Fatma Toufiq ameihoji Serikali kama haioni umuhimu wa kuwaongezea muda wa likizo ya uzazi hadi siku 30 wenza ambao wake zao wamejifungua watoto njia.

Naibu Waziri wa Utumishi, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa wizara hiyo itapokea maoni ya wabunge kuona kama kuna haja ya kubadili kanuni ili kutekeleza ombi hilo.