Rais JOHN MAGUFULI ameiagiza Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano kutangaza tenda ya ujenzi wa barabara ya kiuchumi ya MTWARA-TANDAHIMBA-NEWALA hadi MASASI yenye urefu wa Kilometa MIA MOJA katika bajeti ya mwaka 2019/2020 ambayo awali ilikuwa inajengwa kwa Kilometa HAMSINI.
Rais MAGUFULI amesema hayo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara hiyo ambayo ujenzi wake umekuwa ukisuasua na kuitaka Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano kuacha kuwapa kazi wakandarasi wenye rekodi mbaya katika utendaji wao.
Siku ya PILI ya ziara ya Rais JOHN MAGUFULI Mkoani MTWARA ambapo anaweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kiuchumi ya kutoka MTWARA-TANDAHIMBA-NEWALA hadi MASASI na kusema haridhishwi na kasi ya mkandarasi anayetekeleza mradi huo.
Rais MAGUFULI amesema ujenzi wa barabara hiyo kwa urefu wa Kilometa HAMSINI ambazo zilitarajiwa kukamilika January mwaka huu umekuwa ukisuasua.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini –TANROADS, CYPRIANUS AKO alitoa taarifa ya ujenzi wa barabara huku Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano ISSACK KAMWELWE akisema fedha alizokuwa anadai mkandarasi tayari zimepatikana.