Yanga kutua Algeria kibabe na Boeing Dreamliner

0
952

Yanga SC itatumia ndege ya Serikali aina ya Boeing 787-8 Dreamliner kwa ajili ya safari yake kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akieleza kuwa hatua hiyo ni utekeleza wa ahadi iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ikiwa ni sehemu ya hamasa yake kwa timu hiyo iliyoweka historia Tanzania.

Msigwa amesema ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 260 itaondoka nchini Juni Mosi ikiwa na kikosi hicho pamoja na mashabiki, msafara ambao utaongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pindi Chana, na itarejea nchini Juni 4, 2023.

Taarifa kutoka Yanga SC inaeleza kuwa safari hiyo ya kihistoria itaanza saa 5 asubuhi msafara ukiwa na watu 259, huku wakielekeza shukrani zao kwa Rais Samia kwa hamasa kubwa aliyoionesha kwenye michezo.

Kutokana na kupoteza mchezo wa kwanza kwa magoli 2-1, Yanga itahitaji ushindi wa magoli mawili au zaidi kuweza kurejea na kombe hilo.

Fiston Mayele yeye ananyemelea kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa mashindano hayo, ambapo amefunga jumla ya magoli 13 msimu huu tangu klabu hiyo ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa magoli yanayohesabiwa, ana magoli 7 akiongoza hadi sasa.