Dkt. Mpango ashiriki mkutano wa AfDB

0
317

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema upo umuhimu wa kuboresha utaratibu wa ufadhili wa miradi ya maendeleo na majukumu ya taasisi za fedha za kimataifa, ili kuendana na mabadiliko yaliyotokea duniani tangu kuundwa kwa taasisi hizo.

Makamu wa Rais amesema hayo katika majadiliano ya viongozi wa ngazi ya juu katika mjadala uliohusu ‘Kuboresha utaratibu wa ufadhili wa miradi ya maendeleo na majukumu ya taasisi za fedha za kimataifa’ yaliyofanyika katika mkutano wa mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri.

Amesema taasisi za fedha za Kimataifa ziliundwa kipindi ambacho ni tofauti na sasa ambapo dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali mpya kama vile mabadiliko ya Tabianchi, majanga mbalimbali ya asili, maradhi ya mlipuko, uhaba wa chakula pamoja na migogoro ya Kimataifa na vita.

Aidha, amesema kuongezeka kwa idadi ya watu duniani hususani kwa Bara la Afrika lazima kuzingatiwa katika maboresho ya taasisi za Kimataifa za fedha kwani bado uwakilishi wa Afrika katika taasisi hizo hauendani na idadi ya watu waliopo barani humo.

Makamu wa Rais amesema ni vema katika maboresho ya taasisi za kimataifa za fedha kuweka utaratibu wa kuzingatia vipaumbele vya mataifa husika wakati wa utoaji wa ufadhili pamoja na kuweka mkazo katika malengo ya maendeleo endelevu.

Mkutano huo wa
mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi.