Ramaphosa ashutumu mashambulio kwa wageni

0
508

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameshutumu mashambulio ya hivi karibuni dhidi ya wageni nchini humo na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua wahusika wote.

Katika taarifa yake, Rais Ramaphosa amesema kuwa mashambulio hayo ambayo hasa  yaliwalenga Raia wa Malawi wanaoishi nchini Afrika Kusini pamoja na raia wa Mataifa mengine katika jimbo la KwaZulu-Natal  hayakubaliki.

Rais Ramaphosa amelazimika kutoa kauli hiyo kufuatia tukio la wiki iliyopita ambapo mamia wa raia wa kigeni katika jimbo hilo la   KwaZulu-Natal  walilazimika kuyakimbia makazi yao baada ya watu  wenye hasira kuvamia makazi yao na kuchoma moto maduka.

Amefafanua kuwa, mafanikio ya Afrika Kusini katika uwekezaji yamechangiwa na uhusiano mzuri baina ya nchi hiyo na mataifa mbalimbali, hivyo si vema raia wa kigeni wakashambuliwa kwa kuwa nao ni sehemu ya mafanikio ya nchi hiyo.

Rais huyo wa Afrika Kusini, – Cyril Ramaphosa ameyasema hayo wakati huu ambapo Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa wa nchi hiyo Lindiwe Sisulu akitarajiwa kukutana na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini humo kwa lengo la kujadili mashambulio hayo dhidi ya raia wa kigeni.