Kiswahili chatamba Nigeria

0
348

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana amesema lugha ya Kiswahili inatamba nchini Nigeria kupitia Redio ya Taifa ya Sauti ya Nigeria (VON).

Amesema kwa sasa ubalozi Tanzania nchini Nigeria umeanzisha darasa la Kiswahili kwa watumishi wa VON hasa watangazaji na waandishi wa habari wa idhaa ya Kiswahili.

Dkt. Bana amesema ndani ya kipindi cha miaka minne, Ubalozi wa Tanzania nchini Nigeria umefanikiwa kuchagiza maendeleo ya Kiswahili katika vyuo vikuu pamoja na Shirika hilo la Habari la Nigeria.

Balozi Bana ameyasema hayo wakati wa mazungumzo yake na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt. Ayub Rioba Chacha ambaye yupo nchini Nigeria kuhudhuria kikao cha Umoja wa Vyombo vya Habari Afrika (AUB).

Ameishukuru TBC kwa kushirikiana ubalozi huo katika kufanikisha juhudi za kukuza lugha ya Kiswahili kupitia makubaliano kati ya TBC na VON.

Kwa upande wake Dkt. Rioba amempongeza Balozi Bana kwa jitihada zake za kuitangaza lugha ya Kiswahili kupitia vyombo ya habari na kusisitiza umuhimu wa umoja katika Bara la Afrika.

“Ni suala muhimu ambalo Afrika lilitakiwa lifanyike muda mrefu, mimi sijui ni kwa nini hadi sasa nahitaji Visa,hakuna sababu ya Afrika kuwa na vizuizi vinavyochangia kuchelewesha mambo, ushirikiano huu ni muhimu sana,” Amesema Dkt. Rioba