Chongolo : Muda wa siasa bado

0
191

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amewatahadharisha wanachama wa chama hicho wanaoanza kujipitisha kwa wananchi ili kutaka nafasi za Ubunge na Udiwani waache mara moja.

Amesema wakati wa kufanya hivyo bado, na kwamba kufanya hivyo ni kukiuka taratibu na miongozo ya CCM.

Chongolo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa mikutano wa CCM wilayani Bukombe mkoani Geita na kuweka jiwe la msingi katika nyumba ya kupumzikia wageni, mradi ambao umefikia asilimia 80 ya ujenzi na mpaka sasa umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 200.

“Niwaambie tu muda bado, kwa kufanya hivyo mnakiuka taratibu na kwa kweli tunawaona na tutawachukulia hatua za kinidhamu. Chama hiki kina taratibu zake muda wa siasa bado, sasa hivi waacheni waliopo wafanye kazi ikifika 2025 nafasi zitatangazwa hapo itakuwa ni ruksa kwa kila mwanachama kugombea ila kwa sasa acheni fitna na uchonganishi.” Amesema Chongolo

Aidha, amewataka Watendaji wa halmashauri nchini kote kusimamia fedha za miradi ya maendeleo zilizopelekwa kwenye halmashauri zao.