Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa tatizo la saratani kwa Watanzania linaweza kupungua endapo kutakuwa na tabia ya kupima afya mara kwa mara.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo jijini Dar es salaam mara baada ya kuzindua jengo na mashine mpya za tiba ya mionzi – LINAC katika Taasisi ya Saratani Ocean Road.
Mashine hizo ni za kisasa na kwa Afrika Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa nazo.
“tunaweza kujikinga kwa kufuata kanuni za afya zinavyotuelekeza kula chakula bora, kufanya mazoezi mara kwa mara na kuepuka kunywa pombe kupita kiasi na kuepuka matumizi ya tumbaku”,amesema Makamu wa Rais.
Mradi wa ununuzi na ufungaji wa mashine hizo mpya za kisasa za tiba ya mionzi umegharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali, ambapo Shilingi Bilioni 9.5 zimetumika.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali itaendelea kuimarisha huduma za uchunguzi, matibabu na kinga kwa ugonjwa wa saratani.