Familia zimekumbushwa kujadili masuala ya maadili ili kujiepusha na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayotajwa kukithiri ndani ya jamii katika siku za hivi karibuni
Wito huo umetolewa mkoani Dodoma na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mayamaya wilayani Bahi, ikiwa ni maandalizi ya maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Familia tarehe 15 mwezi huu.
Amesema kasi ya kuporomoka kwa maadili inachochewa na ukuaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo watoto na vijana wamekuwa wakiiga tamaduni na desturi za jamii zingine zinazokinzana na mila na desturi za Mtanzania.
Waziri Gwajima ametaja changamoto za kiuchumi ndani ya familia kuwa chanzo cha mmomonyoko wa maadili, ambapo wazazi au walezi wamejikuta wakitumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi na kusahau wajibu wao wa kusimamia malezi na makuzi yenye maadili mema kwa watoto.
Amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhimiza maadili mema na upendo ndani ya familia, bado kuna matukio mengi ya ukatili dhidi ya watoto katika familia, shuleni na kwenye jamii ikiwemo ukatili mitandaoni.