MCHAKATO WA KATIBA MPYA WAANZA

0
220

Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi, kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama va Siasa.

Lengo la kikao hicho ni kuwashirikisha wadau katika kutathmini utekelezaji wa mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu Chamwino, Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali kuhusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.

Kikao hicho kimejadili namna ya kushirikisha wadau mbalimbali na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka pande zote mbili Tanzania Bara na Zanzibar.

Mbali na mchakato huo wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi zikiwemo Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro na watendaji wa taasisi mbalimbali.