Biashara kati ya Tanzania na Ufaransa imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 27.8 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi Bilioni 94.5 mwaka 2022.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Stergomena Tax amesema hayo mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akifungua mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa.
Amesema mbali na kukua kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili, pia kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Ufaransa ambapo kwa mwaka 2022 Tanzania ilipokea watalii zaidi ya Laki moja kutoka Ufaransa na kuwa nchi ya pili kuleta watalii Tanzania.
“Biashara imeendelea kukua lakini pia katika uwekezaji tunashirikiana, katika utalii Ufaransa imekuwa nchi ya pili kwa kuleta watalii kwenye Taifa letu, haya yanatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan”. Amesema Dkt. Tax na kuongeza kuwa
“Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji na watalii hasa kupitia filamu ya Royal Tour na ndiyo maana utalii umeongezeka,”
Madhumuni ya mkutano huu wa majadiliano ambao ni wa pili kati ya Tanzania na Ufaransa ni kuwawezesha Wafaransa kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana Tanzania pamoja na Watanzania kuzijua fursa zinazopatikana Ufaransa ili kuzitumia kwa maslahi ya pande zote mbili.