Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale imeendelea kuweka mikakati yake ya kuainisha maeneo ya kihistoria yaliyopo wilaya ya Chamwino kwa lengo la kuyatangaza kiutalii ili kwenda sambamba na kasi ya matokeo chanya ya Filamu ya ‘The Royal Tour.’
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale, Dkt. Chistowaja Ntandu alipotembelea Kijiji cha Chamwino kilichopo katika wilaya ya Chamwino kwa ajili ya kubainisha na kukagua maeneo ya kihistoria pamoja na kukutana na baadhi ya wazee ili kupata historia ya eneo hilo adhimu.
Dkt. Ntandu amesema, wilaya ya Chamwino ina utajiri mkubwa wa historia unaoenda sambamba na historia ya Mwasisi wa Taifa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mwl. Julius Nyerere alipopata wazo la kuhamishia makao makuu ya nchi Dodoma, na utekelezaji wa sera ya Ujamaa na Kujitegemea kuanzia mwaka 1969 hadi 1974.
Aidha, Dkt. Ntandu ameeleza kuwa kuna fursa ya kuanzisha makumbusho itakayohifadhi historia adhimu ya Chamwino na kuendeleza utajiri huo kama zao la utalii utakaoendana na kasi ya ongezeko la watalii nchini kama ilivyoelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Hassan Abbas wakati wa maadhimisho ya mwaka mmoja wa matokeo ya Royal Tour.
Katika ziara hiyo, Dkt.Ntandu ametembelea Kisima cha Ipala la Ntembo ambacho kilitumiwa na wananchi kumwagilia bustani za vikundi kabla ya kuanzisha kijiji cha Chamwino, Mti wa Mnyinga uliotumika kwa mikutano, eneo la nyumba kumi za kwanza za kijiji cha Ujamaa.
Maeneo mengine ni pamoja na Nyumba ya Mwasisi wa Kijiji cha Ujamaa cha Chamwino, Mzee Lobinaa, Mesi ya chakula iliyotumiwa na watumishi na wageni wa Ikulu, eneo la Kibaraza (Chibalangu) lililotumika kufyatua matofali ya ujenzi wa nyumba bora, zahanati ya kwanza na ukumbi wa mikutano.