Leo ni siku ya Malaria Duniani, ambapo kitaifa siku hiyo inaadhimishwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Lengo la maadhimisho hayo ni kutoa elimu na hamasa zaidi kwa jamii juu ya kujikinga na ugonjwa wa malaria ili kuepuka madhara yanayatokana na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Malaria, vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua kwa asilimia 76 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 1,502 mwaka 2022 huku waliothibitishwa kuugua Malaria wakipungua kutoka watu milioni 7.7 mwaka 2015 hadi watu milioni 3.5 mwaka 2022.
Nayo maambukizi ya Malaria nchini yamepungua ambapo mwaka 2008 takwimu zilionesha kuwa asilimia 18.1 walikuwa na Malaria ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2022 ambapo kiwango kilikuwa asilimia 8.1.
Awali mikoa sita tu ndio iliyofanikisha kushusha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria, lakini sasa mikoa mitatu ya Songwe, Dar es Salaam na Mwanza nayo imepunguza maambukizi hayo na kufanya idadi ya mikoa hiyo kufikia tisa.