Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa katika kukabiliana na changamoto ya uhaba wa madaktari bingwa katika baadhi ya hospitali za Rufaa za mikoa, wizara hiyo imelenga kugawa upya madaktari bingwa waliopo katika hospitali ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Waziri Ummy amesema hayo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akitoa ufafanuzi zaidi kufuatia swali lililoulizwa na Mbunge wa jimbo la Tabora Mjini Emmanuel Mwakasaka.
“Hatua ya haraka ambayo tumeifanya, tumefanya tathmini ya madaktari bingwa, tumegundua baadhi ya hospitali za Rufaa za Mikoa kuna madaktari bingwa wengi kuliko baadhi ya hospitali nyingine, kwa hiyo tunafanya ugawaji upya ili kukidhi mahitaji katika kila hospitali wakati tunasubiri walioenda kusoma.” Amesema Waziri Ummy
Ameongeza kuwa mwaka huu wizara ya Afya imepata kibali kipya cha ajira, hivyo imelenga kuajiri madaktari bingwa na kuwasambaza katika hospitali za Rufaa za Mikoa hasa zile zenye changamoto ya upungufu ili kukabiliana na changamoto ya wataalamu aina hiyo.
Aidha, Waziri Ummy amesema Serikali inaendelea na mkakati wa kusomesha wataalamu kwa mfumo wa kujiendeleza katika fani za kibingwa na wanapomaliza wanarudi katika vituo vyao ili kuendelea na majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.