Mapigano yaathiri huduma mbalimbali Sudan

0
247

Mashirika ya Kimataifa yanayotoa huduma za afya nchini Sudan yamesema, hospitali ziko hatarini kulemewa na wagonjwa kufuatia kuwepo kwa idadi kubwa ya majeruhi wanaotokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Madaktari pamoja na wauguzi kutoka mashirika hayo likiwemo llile ya Kimataifa la Msalaba Mwekundu wamesema, wamekuwa wakipokea majeruhi wengi kwa siku, huku mazingira ya kuwapatia huduma yakiwa si rafiki hasa katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.

Takribani watu 200 wameuawa na wengine zaidi ya 1,800 wamejeruhiwa nchini Sudan, katika mapigano baina ya Jeshi la nchi hiyo na Wanamgambo wa RSF.

Wakazi wa mji mkuu wa Khartoum na miji mingine kwa sasa
hawana huduma ya umeme pamoja na maji.

Raia wa Sudan wamesema wanahofia usalama wao kwa kuwa Wanajeshi na Wanamgambo wanaopigana pia wanavamia makazi yao.

Wakati mapigano hayo yakiendelea kati ya Jeshi la Sudan na Wanamgambo wa
RSF, Iraq imesema iko tayari kusimamia mazungumzo yenye lengo la kumaliza mgogoro uliopo baina ya pande hizo mbili.