Dkt.Samia : Watanzania changamkieni fursa

0
172

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wakazi wa mikoa ya Morogoro, Lindi na Songwe kuchangamkia fursa ya uwepo wa miradi ya uchimbaji madini ili kujiletea maendeleo.

Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba mitatu ya uchimbaji madini na kampuni tatu kutoka nchini Australia.

Amewataka Watanzania kujipanga kufanya kazi kwa bidii na na kwenda kutoa huduma mbalimbali katika migodi hiyo ikiwa ni pamoja na Mama Lishe kwenda kulisha kwenye migodi.

Kampuni hizo zinakwenda kuchimba madini katika vijiji vya Epanko (Morogoro) ambapo yatachimbwa madini ya kinywe, Chilalo (Lindi) yatachimbwa madini na Kinywe na Ngwala (Songwe) ambapo yatachimbwa madini ambayo ni adimu kupatikana.

Rais Samia amesema utafiti ulioanza kufanyika katika maeneo hayo mwaka 2000 umebaini kuwa, katika kijiji cha Chilalo kuna mashapo yenye tani Milioni 67 za madini ya Kinywe ambayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18 na katika kijiji cha Epanko kuna mashapo yenye tani Milioni 63 za madini ya Kinywe ambayo nayo yatachimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 18.

Tani Milioni 18.5 za madini adimu zimebainika katika kijiji cha Ngwala na madini hayo yatachimbwa katika muda wa zaidi ya miaka 20.

Rais Samia ameongeza kuwa Tanzania itapata faida kubwa kutokana na uchimbwaji wa madini hayo kwa kuwa madini hayo ni ya kimkakati duniani hasa katika teknolojia mpya za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ambapo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na mitambo.