Simba: Tumeshinda mechi ngumu, hatuishindwi Yanga

0
512

Afisa Habari wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa, timu hiyo hupata ushindi kwenye mechi ngumu zaidi, hivyo haiwezi kushindwa kuifunga Yanga SC.

Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam kuelekea mchezo huo amesema, kwao huo ni mchezo mkubwa sana, na lazima wachezaji wao wajue wana kazi kubwa ya kuwarudishia furaha mashabiki kwenye Kariakoo Derby.

“Tunao watu wa kutuvusha salama kwenye mchezo huu. Ni wakati wao wachezaji kuandika historia kubwa kwenye Kariakoo Derby,” amesema Ally.

Amewasihi mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani akisema “kama menejimenti tunafanya kila kitu kwa upande wetu kuhakikisha tunapata ushindi, na nyie kama mashabiki fanyeni jukumu lenu kwa kununua tiketi na kuja uwanjani kushangilia timu yenu.”

Mchezo huo wenye msisimko wa aina yake katika soka la Tanzania utapigwa Aprili 16, 2023 saa 11:00 jioni, ambapo Yanga inataka kuendeleza ubabe na kutetea ubingwa wa ligi, huku Simba ikitafuta kufuta uteja huo, na kuhakikisha licha ya kuwa uwezekano wa kushinda ligi ni mdogo, basi wasifungwe.