Frank Lampard ameteuliwa kuwa kocha wa muda wa Chelsea FC ambapo atainoa timu hiyo hadi mwisho mwa msimu.
Lampard anarudi tena Darajani kama kocha baada ya kuitumikia kwa mafanikio akiwa mchezaji akishinda mara tatu Ligi Kuu ya England pamoja na taji moja la UEFA.
Kati ya Julai 2019 hadi Januari 2021 alikuwa kocha wa The Blues akiiongoza katika michezo 84, akishinda michezo 44, akitoka sare 17 na kupoteza 23.
Lampard ana kibarua cha kuwapandisha Chelsea kutoka nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi lakini pia kuwaongoza katika mchezo wa robo fainali wa Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid.
Aprili 2 mwaka huu Chelsea ilivunja mkataba na Graham Potter kutokana na matokeo yasiyorodhisha, na sasa itakuwa katika kibarua cha kutafuta kocha wa kudumu.