Maagizo ya Waziri Mkuu kwa Makatibu Tawala

0
181

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuna ushirikishwaji wa karibu wa Wananchi katika kuainisha changamoto zinazowakabili pamoja na kuwawezesha kutekeleza afua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hizo.

Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa chama cha Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halamashauri jijini Dodoma Waziri Mkuu amesema, kwa kufanya hivyo Serikali itaweza kutekeleza tija ya dhana ya ugatuzi wa madaraka pamoja na kuhakikisha kuwa maendeleo endelevu ni dhahiri yanapatikana kwa Wananchi.

Amewakumbusha viongozi hao kuhakikisha suala la ulinzi na usalama linakuwa kipaumbele katika maeneo yao ya kazi na utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji unaendelea kuwa agenda itakayobebwa kwa uzito katika jamii.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amewaelekeza Viongozi hao kusimamia makusanyo ya fedha za Serikali na kusimamia mienendo ya kiuchumi katika mamlaka zao ili kusaidia kujenga miradi ya maendeleo katika maeneo yao.