Rosela kutibu unene uliopita kiasi

0
254

Kupitia tafiti iliyochapishwa katika jarida la Kimataifa la Sayansi ya Chakula na Teknolojia, mmea wa Rosela umeelezwa kuwa na uwezo wa kutibu tatizo la unene uliopita kiasi (obesity).

Kwa mujibu wa takwimu kutoka shirika la afya duniani katika idadi ya watu bilioni nane duniani inakadiriwa kuwa zaidi ya watu zaidi bilioni 2.3 ikiwemo watoto na watu wazima wanauzito uliopitiliza ambapo hadi kufikia 2030 inakadiriwa mwanamke mmoja katika watano na mwanaume mmoja katika saba watakuwa wanaishi na tatizo la unene uliopita kiasi.

Tatizo hilo linaelezwa kuweza kudhibitika kwa njia za kubadilisha mtindo wa maisha kama vile kuwa na mpangilio mzuri wa chakula na ule wa mazoezi ya mimwili.

Hata hivyo timu ya wanasayansi kutoka nchi ya Australia wamefanya utafiti na hatimae kuja na suluhisho la tatizo hilo la unene uliopita kiasi.

Wanasayansi hao wamechunguza aina ya mauwa maarufu Rosela (hibiscus) na kugundua kuwa yanaweza kutumika kama sehemu ya tiba ya unene uliopita kiasi.

Timu hiyo iliyoongozwa na mwanafunzi wa shahada ya juu ya udaktari (Ph.D) Manisha Singh kutoka chuo kikuu cha RMIT huko Melbourne imechukua sampuli kutoka katika ua la rosela (hibiscus sabdariffa) na kuchunguza uwezo wake wa kuzuia seli za mafuta kujilimbikiza mwilini.

Mbinu zilizotumika na timu hiyo zimehusisha kuchunguza uwezo wa kuzigeuzwa seli kabla hazijabadilishwa kuwa mafuta kwa kutumia aina mbili za chemikali ambazo ni hydroxycitric na Phenolic ambazo zinatokana na mmea wa Rosela.

Matokeo ya tafuti hizo ni kuwa seli zilizotibiwa na kemikali ya asidi ya hydroxycitric hazikuonesha mabadiliko yotote ya kubadilika kwa kiwango cha mafuta katika seli hizo wakati seli zilizotibiwa na phenolic zimeonesha kuwa na asilimia 95 upungufu wa mafuta hivyo kuweka tafsiri kuwa phenolic imekuwa na ufanisi mkubwa katika kudhibiti ulimbikizaji wa mafuta mwili.

Timu hiyo ya utafiti imeeleza kuwa matokeo ya utafiti huo yanaweza kuiongoza jamii kwa namna ambavyo imekuwa ikikabiliana na tatizo la uzito uliokithiri kwani pamoja na kuwa matibabu yakiyopo hivi sasa yanaonekana kuwa na ufanisi ila moja ya athari zake yanaweza pelekea matatizo mengine ya kiafya kama shinikizo la damu, matatizo ya figo na ini.

Vilevile timu hiyo imeeleza kuwa phenolic kutoka katika mmea wa Roselle inaweza kutumika kutengeneza bidhaa za vyakula ambazo zitakuwa na ufanisi katika kuingilia kati uundaji wa seli za mafuta mwilini.

Hatua inayofuata baada ya utafiti huo ni timu hiyo kuhifadhi phenolic kutoka kwenye mmea ili zitumike katika bidhaa za vyakula na hata kutengeneza vinywaji.