Moja ya viungo bora katika soka, Mesut Ozil ametangaza kustaafu soka akiwa na umri wa miaka 34.
Ozil ambaye amezichezea Real Madrid na Arsenal ameshinda mataji tisa katika maisha yake ya soka, na pia ameichezea Ujerumani michezo 92, akiwa sehemu ya timu iliyoshinda Kombe la Dunia mwaka 2014.
“Imekuwa safari bora sana ikiwa imesheheni kumbukumbu na hisia mchanganyiko zisizofutika,” amesema akitangaza kustaafu baada ya miaka 17 ya soka la kulipwa.
Safari yake ilianzia Schalke na Werder Bremen kabla ya kutimkia Hispania mwaka 2010 na kwenda England mwaka 2013.
Januari 2021 alijiunga na Fenerbahce akiwa mchezaji huru, lakini walifikia makubaliano ya kusitisha mkataba Julai 2022, kisha akajiunga na Basaksehir ambako alicheza michezo nane tu kutokana na majeraha.
Raia huyo wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ujerumani mara tano.
Alitangaza kustaafu soka la kimataifa mwaka 2018 kutokana na kile alichosema ni ubaguzi wa rangi na kutoheshimiwa.