Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Geita, Nicolaus Kasandamila amesema chama hicho kitafuatilia fedha zote zilizotolewa na mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM) kwenye halmashauri za mkoa huo kama sehemu ya msaada kwa jamii
(CSR).
Kasandamila amesema
Wenyeviti wote wa halmashauri mkoani Geita wameahidi kusimamia fedha hizo na kwamba miradi iliyolengwa itamalizika kwa wakati, hivyo jukumu la CCM ni kufuatilia ahadi hizo kwenye maeneo ya Wananchi.
Amesema fedha zinazotolewa ni nyingi, hivyo kila halmashauri inapaswa kutekeleza miradi iliyokusudiwa na matokeo ya miradi hiyo ionekane na sio maneno matupu.
Mwenyekiti huyo wa CCM mkoani Geita amezionya halmashauri zote za mkoa huo kutotumia fedha za miradi ya kijamii kinyume na malengo yaliyoainishwa kwenye maeneo hayo.
GGM imetoa shilingi Bilioni 19 kwa halmashari tano za mkoa wa Geita ikiwa ni sehemu ya mchango wake kwenye kusaidia jamii ya halmashauri hizo.