Serikali yatoa mitambo ya kuchimba visima vijijini

0
189

Serikali imekabidhi mitambo ya uchimbaji visima kwa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na kuutaka wakala huo kuitumi katika matumizi yaliokusudiwa ikiwemo kutoa huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu.

Rai hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akikabidhi mitambo hiyo, zoezi lililofanyika wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa RUWASA kwa mwaka 2021/2022 jijini Dar es Salaam.

Ameiagiza RUWASA kutambua wanapaswa kutoa huduma zaidi kwa wananchi kuliko kufanya biashara, hivyo ametaka kufanyika tathmini ya bei wanazotoza kuchimba visima binafsi vya wananchi ili kuhakikisha haziwi juu zaidi ya bei za kampuni binafsi.

Katika hatua nyingine ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuongeza nguvu katika kufanya ukaguzi wa ankara za maji zinatolewa kwa wateja wa mamlaka za maji zote nchini na zile zitakazobainika kukiuka utaratibu uliowekwa zishughulikiwe kwa mujibu wa taratibu ikiwemo mamlaka zote za maji ambazo zinatoza bei ambazo hazijaidhinishwa na EWURA.

Awali, Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi amesema amesema baadhi ya mamlaka za maji zimepunguza utegemezi kwa serikali kwa kulipia gharama za uendeshaji na kutumia mapato ya ndani na mikopo kutekeleza miradi mikubwa ya maji ya kuongeza upatikanaji wa majisafi katika maeneo ya miji wanayoisimamia.