Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kutekeleza miradi mipya na ile ya zamani, ili kuwaletea Wananchi maendeleo.
Dkt. Samia ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akihutubia sherehe maalum za kumpongeza kwa kutimiza miaka miwili ya uongozi wake, sherehe zilizoandaliwa na Umoja wa Wanawake wa Tanzania (UWT).
Amesema miradi iliyoibuliwa na Serikali ya awamu ya Tano inaendelea kutekelezwa ukiwemo ule wa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 za umeme na mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
Kuhusu sekta ya Kilimo Dkt. Samia amewataka vijana nchini kujiajiri katika sekta hiyo badala ya kuwaachia wazee.
Rais Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa Rais wa awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano Dkt. John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.