Tanzania imejipanga kuzalisha chakula cha kutosha, ili kukabiliana na upungufu wa chakula nchini.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa maandalizi ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani ya Kilimo Afrika (AGRF) linalotarajiwa kufanyika nchini Septemba 5 hadi 8 mwaka huu, Rais Samia amesema Tanzania imejipanga kuwa ghala la chakula Barani Afrika ili kukabiliana na utegemezi wa chakula kutoka nje ya bara hilo.
Rais Samia ameongeza kuwa Tanzania imedhamiria kukabiliana na upungufu wa sukari nchini, ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara.
Wakati wa uzinduzi huo wa maandalizi ya Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani ya Kilimo Afrika, Rais Samia ameongoza harambee ya kuchangia Mfuko wa Kilimo wenye lengo la kusaidia kuwainua Wanawake na Vijana.
Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa
Jukwaa la Mapinduzi ya Kijani ya Kilimo Afrika kutokana na hatua ilizochukua za kufanya mageuzi katika sekta ya kilimo tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.
Hatua hizo ni pamoja na kuongeza bajeti katika wizara ya Kilimo ili kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo za ugani na upatikanaji wa mbolea.