Timu ya Nkana FC ya Zambia anayochezea Mtanzania Hassan Ramadhani Kessy itamenyana na CS Sfaxien ya Tunisia katika Robo Fainali ya kombe la shirikisho mwezi Aprili mwaka huu.
Katika droo iliyopangwa usiku wa jana, Nkana FC itaanzia nyumbani mjini Kitwe Aprili Saba kabla ya kwenda Tunis Aprili 14 kwa mchezo wa marudiano.
Mechi nyingine za Robo Fainali Kombe la Shirikisho, Etoile DU Sahel ya Tunisia itamenyana na AL Hilal ya Sudan wakati Hassania Agadir wakianzia nyumbani dhidi ya Zamalek ya Misri huku Gor Mahia ya Kenya wakikabiliwa na kibarua cha kumenyana na RS Berkane ya Morocco.
Endapo Nkana FC itatinga hatua ya nusu fainali, itamenyana na mshindi kati ya Gor Mahia na RS Berkane, wakati mshindi kati ya Etoile DU Sahel na AL Hilal atamenyana na mshindi kati ya Hassania Agadir na Zamalek, na mechi za kwanza za nusu fainali zitachezwa Aprili 28 na marudiano itakuwa ni Mei 5 mwaka huu.
Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho msimu wa 2018/2019 itachezwa Mei 19 na marudiano yatakuwa Mei 26.