Meneja wa wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) mkoa wa Mwanza Mhandisi Geofrey Sanga amesema Serikali ya awamu ya sita imeongeza bajeti ya wakala huo kutoka shilingi Bilioni 23 hadi kufikia shilingi Bilioni 197, ili kuiwezesha kutekeleza miradi ya maji vijijini katika mkoa huo.
Akitoa taarifa ya mafanikio ya RUWASA mkoa wa Mwanza Mhandisi Sanga amesema, ongezeko hilo la fedha litawawezesha kuhudumia Wananchi wengi zaidi na kwenye maeneo ya vijijini.
Mhandisi Sanga amesema, wanatarajia kufikia lengo la kumtua Mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2025 kwa kupeleka maji katika maeneo yote ya vijijini kutokana na miradi inayoendelea kutekelezwa hivi sasa.
Ameongeza kuwa mkoa wa Mwanza umepokea mtambo wa kuchimba visima virefu ambao utaharakisha kazi ya kuchimba visima na kusambaza maji kwa Wananchi kwenye maeneo ya karibu zaidi.