Wanawake washerehekea siku yao

0
112

Leo ni Siku ya Wanawake Duniani, ambapo Wanawake hapa nchini wanaungana na wenzao wa mataifa mbalimbali kusherehekea siku hiyo.

Harakati za kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake Duniani zilianza mwaka 1908 wakati takribani Wanawake elfu 15 waliandamana katika jiji la New York, Marekani kudai muda mfupi wa kazi, mishahara bora na haki ya kupiga kura.

Mwaka mmoja baadaye chama cha Kisoshalisti cha Marekani kilitangaza Siku ya Kitaifa ya Wanawake ya kwanza na wazo la kuifanya siku hiyo kuwa ya kimataifa lilitoka kwa Clara Zetkin, mwanaharakati wa Kikomunisti na mtetezi wa haki za Wanawake.

Alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 wakati wa mkutano wa kimataifa wa Wanawake wafanyakazi huko Copenhagen, ambapo Wanawake 100 walioshiriki katika mkutano huo kutoka nchi 17 walikubali pendekezo lake.

Siku ya Wanawake Duniani iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1911 katika nchi za Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi na maadhimisho ya mwaka huu ni ya 111.