TANESCO yapanda miti Kilolo

0
203

Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani hapo kesho, Jukwaa la Wanawake la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limepanda miti zaidi ya 500 wilayani Kilolo mkoani Iringa, lengo likiwa ni kulinda vyanzo vya maji ambavyo ni muhimu kwenye uzalishaji wa umeme.

Kampeni hiyo imezinduliwa na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Anna Msola ambaye amepongeza jitihada zilizofanywa na TANESCO kuhakikisha inalinda vyanzo vya maji.

Msola amesema mito mingi iliyopo wilayani Kilolo inatiririsha maji yake kwenye mto Ruaha Mkuu ambao ndio chanzo kikubwa kinachopeleka maji kwenye mabwawa ya kufua umeme.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Meneja wa TANESCO wilaya ya Kilolo Mhandisi Mwamvita Ally amesema, kampeni hiyo ya Panda miti, mvua ndii, umeme ndindindiiiii, ina lengo la kupanda miti kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wanawake la TANESCO Prisca Maziwa amelishukuru shirika hilo kwa kuwaruhusu wanawake kuendesha kampeni hiyo, kwani miongoni mwa vipaumbele vya shirika hilo ni kutunza mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji.