Ajali yaua watatu Chalinze

0
194

Watu watatu wamefariki dunia na mwingine mmoja amejeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea mkoani Pwani baada ya gari dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Chalinze kwenda Lugoba kugonga karavati na kupinduka katika kijiji cha Mboga kilichopo katika halmashauri ya Chalinze.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema ajali hiyo imehusicha gari dogo aina ya Toyota Crester lenye namba za usajili T 323 BAL.

Amewataja waliofariki dunia katika ajali hiyo kuwa ni dereva aliyekuwa anaendesha gari hilo Mkaguzi msaidizi wa polisi Ndwaga Dastani (28), konstebo wa polisi Emiliana Charles (26) wote askari polisi wa kituo cha polisi Chalinze na Karim Simba (27) mfanyakazi wa mahakama ya Lugoma.

Kamanda Lutumo amesema majeruhi wa ajali hiyo konstebo wa polisi Mwanaidi Shabani amepelekwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam na maiti zimehifadhiwa katika kituo cha afya Lugoba.

Amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo lililopata ajali.