Nguvu ya mitandao ya kijamii

0
168

Mitandao ya kijamii inaweza kutumika kama vyombo vya habari vyenye kujenga au kubomoa ukweli hata taswira ya mtu kwenye jamii.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha wakati akiitambulisha mada yake katika kongamano la kukichambua kitabu cha “Continuity with Vision: The Roadmap to Succes for President Samia Suluhu Hassan” (Muendelezo wa Maono katika Safari ya Mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Dkt. Ayub Rioba Chacha ametolea mfano baadhi ya mambo ambayo mitandao ya kijamii ilipotosha umma hadi kuamini kile kinachozushwa kuliko ukweli wenyewe hasa wakati wa janga la UVIKO 19 na kifo cha Rais wa awamu wa tano Dkt. John Magufuli.

“Mtu anaweza akaamua kuua jina lako kwenye mitandao ya kijamii, vuruga kabisa, heshima yako anaondoa kabisa, unabaki hauna maana,” amesema Dkt. Rioba na kuongezea kuwa ipo haja ya kutafuta namna bora ya kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ili kuepuka athari zake kwenye jamii na dunia kwa ujumla.

Katika kitabu hicho chenye sura 29 kilichoandikwa na Wanazuoni wengi, Dkt. Rioba ameandika sura ya nne yenye kichwa cha habari, “The Advent of Online Media in Africa: A Rescue Ship to Freedom or a Trojan Horse of Fake News? A Glimpe into the Tanzanian Experience.” (Ujio wa Vyombo vya Habari Mtandaoni barani Afrika: Meli ya Uokoaji kuelekea Uhuru au Kivuli cha Habari za Uongo? Taswira ya Tajriba ya Tanzania).