Ndejembi atoa siku 60 shule ya wasichana kukamilika

0
170

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Deogratius Ndejembi ametoa muda wa miezi miwili kwa Mkurungenzi wa halmashauri ya Manyoni mkoani Singida kukamilisha ujenzi wa miundombinu yote ya shule maalum ya sayansi ya wasichana ya mkoa huo.

Ndejembi ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ya sayansi yenye kidato cha kwanza hadi cha sita inayojengwa Solya wilayani Manyoni kwa gharama ya shilingi bilioni tatu.

Wakati wa ziara yake Naibu Waziri Ndejembi amebaini mapungufu katika usimamizi wa ujenzi wa shule hiyo ikiwa ni pamoja na kutofuatwa mwongozo wa manunuzi na taratibu za malipo kwa wakandarasi wanaoendelea na ujenzi.

Kufuatia hali hiyo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) wilayani Manyoni kufanya uchunguzi ndani ya kipindi cha siku 7 na kuwasilisha taarifa yake TAMISEMI ili hatua stahiki zichukuliwe.

Pia Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI amemuagiza Mkurungenzi wa halmashauri ya Manyoni kuwachukulia hatua za kinidhamu Afisa Manunuzi na Mhandisi anayesimamia ujenzi wa miundombinu katika shule hiyo maalum ya sayansi ya wasichana mkoani Singida
kwa kufanya malipo kwa wakandarasi kinyume na taratibu.