Dodoma inaandika historia kwenye kilimo

0
151

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha kilimo cha umwagiliaji mkoani humo, kitakachowasaidia wakazi wa mkoa huo na Watanzania wote.

Senyamule ameyasema hayo jijini Dodoma alipokua akifungua kongamano la kukichambua kitabu cha “Continuity with Vision: The Roadmap to Succes for President Samia Suluhu Hassan” (Muendelezo wa Maono katika Safari ya Mafanikio ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Amejua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa Watanzania wengi na sisi Dodoma asilimia 72 tunategemea kilimo. Kilimo tunachokitegemea ni cha mvua, na mvua ni chache Dodoma. Mheshimiwa Rais [Samia] ameanzisha kilimo cha umwagiliaji ambacho kitamkomboa Mwanadodoma na Watanzania wengine. Hao ndio watu wenye maono makubwa,” amesema Senyamule

Aidha, ameongeza kuwa Dodoma ina uwezo wa kulima mara tatu hadi nne kutokana na miradi ya ujenzi wa mabwawa ambayo mawili tayari yamekamilika katika wilaya za Mpwapwa na Chamwino.

Mkuu huyo wa mkoa wa Dodoma amewapongeza Wanazuoni walioshiriki kuandika kitabu hicho na kusema kuwa ni jambo kubwa na utashi kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwatumikia Wananchi.