Kiki za malkia wa Sungura

0
343

Wewe kama unadhani kiki zilianza jana au juzi, mpwa unajidanganya.

Kiki zilianza karne nyingi nyuma na pengine hujawahi kumsikia Malkia wa Sungura, Mama aliyefanikiwa kuingia kwenye rekodi ya dunia kwa kusuka mkasa wa kipekee.

Anaitwa Mary Toft, pamoja na mumewe Joshua Toft walifanikiwa kupata watoto 15 wa ajabu chini ya uangalizi wa madaktari na leo hii kutokana na ushuhuda huu Toft ameandikiwa riwaya na kutengenezewa filamu kutukuza uwezo wake wa kutengeneza kiki.

Nikujuze kwamba mara zote Mary alipoenda kujifungua watoto hao hawakuwa watoto bali Sungura, Sungura 15.

Filamu ya Velvet City

Kuna msemo wa kiingereza unaoitwa ‘Maternal impression’ ukiwa na maana kuwa mawazo ya mama mjamzito kuhusu mtoto aliyepo tumboni yanaweza kumgeuza mtoto yule kuwa kile anachokiwaza ama kiuhalisia, na ndicho Mary alichosema kilimkuta kwenye karne ya 18 kati ya mwaka 1720 hadi 1763.

Mwaka 1720 Mary aliolewa na Joshua na Septemba 27, 1726 akiwa ni mama wa watoto wawili aliwashangaza madaktari na wakunga baada ya kushikwa na uchungu na kuanza kujifungua vitu visivyo vya kawaida ikiwemo kichwa na miguu ya paka pamoja na viungo vya wanyama mbalimbali na sungura 15 waliokufa.

Alisema kuwa alikutana na sungura aliyemshtua sana shambani na picha ya sungura yule haikuwahi kutoka kichwani kwake na alijikuta akitaka kula vyakula vyenye nyama ya sungura kila mara na hivyo daktari John Howard aliiamini hadithi yake.

Habari za Mary zilimfikia Mfalme George I na alimtuma daktari wake kuchunguza. Daktari alifika na kumkuta Mary akiwa na uchungu akimalizia kujifungua sungura wa 15 naye akawa na uhakika kuwa hakuna namna hali hii ikawa ni uongo na akachukua baadhi ya watoto wake kwenda London ili kuwaonyesha mfalme na Mwanamfalme wa Wales.

Daktari wa upasuaji aliitwa kufanya upelelezi zaidi na kugundua kuwa kinyesi cha sungura mmoja kilikuwa na punje ya hindi na isingewezekana kuwa sungura hao walikuwa ndani ya tumbo la Mary.

Wakati huohuo, Mary aliendelea kujifungua vitu visivyo vya kawaida ikiwemo miguu ya paka na kibofu cha nguruwe.

Za mwizi 40, hatimaye mtu akakamatwa akiingiza sungura kwenye chumba cha Mary.

Mary alikiri kuwa alishirikiana na mumewe kununua nyama buchani na kujiwekea pamoja na kujiwekea sungura hao waliokufa.

Alikaa jela kwa miezi kadhaa na kibarua cha daktari wa mfalme aliyeamini uongo ule kikaota nyasi.

Mary aliandikiwa kitabu kiitwacho ‘Mary Toft:The Rabbit Queen’ na filamu ya ‘Velvet Cry’