Bilioni 153.56 zashushwa Ngara

0
286

Mkataba wa mradi wa ukarabati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo kwa kiwango cha lami umesainiwa leo wilayani Ngara mkoani Kagera.

Ukarabati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo yenye urefu wa kilomita 92 ni moja ya miradi inayotekelezwa kwa kugharamiwa na Benki Dunia kupitia programu ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP).

Mradi huo unategemewa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 24, na barabara hiyo itakarabatiwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kwa gharama ya shilingi bilioni 153.56 bila kujumuisha VAT ya shilingi bilioni 27.64

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa mradi huo waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema, barabara hiyo ni kiungo muhimu katika nchi za Afrika Mashariki kwa usafirishaji wa bidhaa za nchi za Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Uganda zinazokwenda na kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.

Amesema kukamilika kwake kutarahisisha usafirishaji na hata kukuza uchumi na pia itatoa mchango mkubwa katika shughuli za utalii katika Mbuga za Taifa za Burigi na Rubondo katika mikoa ya Kagera na Geita.
 
Profesa Mbarawa ametoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano katika ulinzi wa mradi na vifaa vitakavyotumika katika ujenzi huo, huku akisisitiza wananchi wanaozunguka eneo la mradi kuepuka uhalifu wa namna yoyote wa vifaa vya ujenzi.