Soko la Madini lafunguliwa Geita

0
338

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya kuwa serikali itamchukulia hatua za kisheria mtu yeyote atakayekamatwa anatorosha Madini.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo mkoani Geita wakati akifungua soko la Madini la mkoa huo.

Amesema kuwa miongoni mwa hatua zitakazochuliwa kwa mtu anayetorosha Madini ni kutaifishiwa Madini aliyokuwa akiyatorosha.

Waziri Mkuu pia amewaagiza viongozi na watendaji wote wa serikali kusimamia kwa weledi, uaminifu na uadilifu, sheria, kanuni na miongozo kuhusu sekta ya Madini kwa lengo la kudhibiti utoroshwaji wa Madini hususani dhahabu kwenda nje ya nchi.

Ameitaka wizara ya Madini, Tume ya Madini Nchini, Uongozi wa mkoa wa Geita, Idara na Taasisi nyingine za serikali zinazohusika na maendeleo ya sekta ya Madini, kuheshimu mipaka ya majukumu yao ili waweze kulisimamia vizuri soko hilo la Madini ili liweze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa.

“Wizara ya Madini ishirikiane na vyama na mashirikisho ya wachimbaji na wafanyabiashara wa Madini katika kuandaa mpango kazi mahsusi kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu ya soko hili ili lisigeuke kuwa kikwazo kipya kwa wachimbaji na wafanyabishara wa Madini”, amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Ufunguzi wa soko hilo la Madini la mkoa wa Geita ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli alilolitoa mwezi Januari mwaka huu la kuitaka mikoa yote nchini ianzishe masoko ya madini.