Mashabiki wa Simba wakiwa hawajasahau changamoto waliyokumbana nayo kupata jezi za klabu yao kwa msimu wa mwaka 2022/23 kutokana na jezi hizo kuchelewa kufika, huenda hali hiyo ikajirudia katika jezi za mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.
Michezo ya makundi ikiwa imeanza, na tayari Simba ikiwa imeshuka dimbani mara moja ugenini, huku Februari 18 ikiwa nyumbani kuikaribisha Raja Casablanca ya Morocco, bado jezi hizo hazijafika.
Akizungumzia hilo Afisa Habari wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa “kutokana na sherehe za mwaka mpya China usafirishaji mizigo ulikuwa wa kusuasua ikabidi Vunjabei aende China kuhakikisha Jezi hazichelewi, ila zikaja kukwama Ethiopia kwa sababu ya ndege za mizigo kuchelewa.”
Hata hivyo amewatoa hofu mashabiki wa Simba kuwa jezi hizo ambazo mashabiki wanazisubiri kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa wiki, zitawasili nchini kabla ya siku ya mchezo huo.
Hata hivyo, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii waliotoa maoni yao kuhusu suala hilo wamekosoa wakisema jambo hili linajirudia mara ya pili, hivyo timu lazima ichukue hatua kukomesha ucheleweshaji wa jezi.