Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itafanya uchunguzi kwa vyama vya msingi vya Ushirika (AMCOS) wilayani mbozi mkoani Songwe na watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wowote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Majaliwa ameyasema hayo baada ya Mbunge wa jimbo la Mbozi, George Mwanisongole kuzilalamikia AMCOS za wilaya hiyo kuwanyonya wakulima wa kahawa na hivyo kuwafanya wauchukie ushirika.
Akizungumza na wananchi katika eneo la Mlowo wilayani Mbozi akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Songwe, Waziri Mkuu amesema ni lazima mwenendo wa AMCOS za Mbozi uchunguzwe kwa manufaa ya wanaushirika wote.
“Ushirika ni muhimu kwa maendeleo ya wakulima lakini wanahitajika wanaushirika waaminifu, hivyo tutakuja kufanya uchunguzi wa mwenendo wa AMCOS za Mbozi ili kubaini wabadhirifu na kuwachukulia hatua. Pia tutachunguza makato wanayokatwa.” amesema Waziri Mkuu