Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yamepaa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 huku serikali ikitumia zaidi ya shilingi Trilioni 19.46 katika matumizi ya kawaida na matumizi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuendelea kwa ujenzi wa miradi ya kimkakati.
Akitoa hotuba ya kuahirisha mkutano wa kumi ya Bunge mkoani Dodoma, Waziri Mkuu amesema shilingi Trilioni 12. 29 zimepelekwa katika matumizi ya kawaida huku zaidi ya shilingi Trilioni 7 zikipelekwa katika shughuli za maendeleo.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema, makusanyo hayo yanatokana na fedha za makusanyo ya ndani shilingi Trilioni 13.40 ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya shilingi Trilioni 11.68 sawa na asilimia 98 ya lengo la kukusanya kodi.
Amesema upatikanaji wa fedha hizo umeiwezesha serikali kukamilisha masuala kadhaa ikiwa ni pamoja uendelezaji wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa Kufua Umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHPP), ujenzi wa mji wa Serikali Mtumba, kugharamia na kukamilisha zoezi la Sensa na uendelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi.
Kutokana na makusanyo na utekelezaji wa miradi hiyo, katika kipindi hicho cha nusu mwaka uchumi wa Taifa umekua kwa asilimia 5.2.