Wabunge, Mawaziri watakiwa kutumia lugha ya staha

0
179

Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson ameamuru kufutwa katika taarifa rasmi za Bunge maneno aliyotamka Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba katika kikao cha pili cha mkutano wa 10 wa Bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania wakati akichangia taarifa za kamati za kudumu za bunge za Ardhi, Maliasili na Utalii na kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.

Spika Tulia amenukuu maneno aliyoyatoa Dkt. Nchemba “Hebu tujadili mambo mengine kuhusu uganga huko ila kuhusu uchumi this is my profession” na kuamuru yafutwe kwenye taarifa rasmi za Bunge na yasiwe rejea katika michango ya wabunge.

Dkt. Tulia amesema, kwa mujibu wa kanuni ya 71 ya kanuni za Bunge ya mwaka 2020 maneno hayo hayana staha na yalimlenga Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina lakini yakachukuliwa kama amewajibu wabunge wote.

Akihitimisha hoja hiyo Spika wa Bunge amewataka wabunge kuchangia hoja zao kwa staha na pia mawaziri wajibu hoja za wabunge kwa staha badala kutoa lugha za kushambuliana binafsi.