Halmashauri zitenge fedha za mpango wa matumizi ya ardhi

0
153

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange amezitaka halmashauri za wilaya zote nchini kutenga fedha kila mwaka katika bajeti zao kwa ajili ya kuandaa Mipango ya Matumizi ya Bora Ardhi kwenye maeneo yote ya vijiji.

Pia amezitaka halmashauri hizo kuweka alama zinazoonekana kwa urahisi ili kuwezesha maeneo hayo kulindwa na kuzuia mwingiliano wa kimatumizi unaofanywa na wananchi.

Dkt. Dugange ametoa agizo hilo Bungeni mkoani Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane aliyetaka kujua Je, ni lini serikali itatekeleza Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kilwa?.

Dkt. Dugange amesema ili kuondoa na kumaliza kabisa migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikijitokeza mara kwa mara, serikali imejipanga kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 6 kwa kila mwaka.