Nkasi kumegewa hekta elfu 10 za hifadhi ya msitu wa Loasi

0
228

Wananchi wa halmashauri ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wanatarajiwa kumegewa hekta 10,828 kutoka katika msitu wa hifadhi wa Loasi, kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani kuhusu mkakati wa serikali wa kuwapatia wananchi maeneo ya kulima kutoka kwenye mapori na hifadhi ambazo hazina wanyama.

Amesema kufuatia uamuzi huo wa Baraza la Mawaziri, wilaya ya Nkasi inatakiwa kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kukidhi mahitaji ya wananchi kwa sababu wilaya hiyo haina uhaba wa maeneo bali ina changamoto ya mgawanyo na mtawanyiko wa makazi na shughuli za kibinadamu.

Aidha, Masanja amekemea tabia ya baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi na kujichukulia sheria mkononi kwa kuwadhuru wahifadhi wanaolinda rasilimali za Taifa.